• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

Mtwara wahimizwa kuzingatia elimu kwa wenye ulemavu

 

Mkurugenzi wa MERODI Frances Chiwango akiwa na wadau wa elimu wakizungumzia umuhimu wa elimu kwa wenye ulemavu(Picha na Musa Mtepa)

Wazazi na walezi mkoani Mtwara wametakiwa kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu katika kipindi hiki cha uandikishaji wa Elimu ya Awali na Msingi. Wito huo umetolewa na MERODI kupitia Jamii FM, ikisisitiza elimu jumuishi, ushirikiano wa jamii na msaada wa serikali kwa wazazi wa watoto wenye ulemavu

Na Musa Mtepa

Wazazi na walezi mkoani Mtwara wametakiwa kuweka kipaumbele katika elimu kwa watoto wenye ulemavu kwa kuhakikisha wanawaandikisha katika kipindi hiki cha uandikishaji wa Elimu ya Awali na Msingi kinachoendelea kote nchini.

Wito huo umetolewa leo Januari 29, 2026 na Frances Chiwango, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na watu wenye ulemavu mkoani Mtwara ya Mtwara Economic Rights Organization for Disabled (MERODI), alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio.

Akizungumza katika kipindi hicho, Chiwango amesema licha ya kuwepo kwa mwamko kwa baadhi ya wazazi na walezi ikilinganishwa na miaka ya nyuma, bado juhudi zaidi zinahitajika ili kuendelea kuwahamasisha wazazi kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu.

Sauti ya 1 – Frances Chiwango, Mkurugenzi wa MERODI

Aidha, Chiwango amesema uamuzi wa serikali kuweka mkazo katika elimu jumuishi umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza unyanyapaa kati ya wanafunzi wenye ulemavu na wasio na ulemavu, akitolea mfano safari yake ya kwanza kuelekea shuleni.

Sauti ya 2 – Frances Chiwango, Mkurugenzi wa MERODI

Vilevile, ametoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa pamoja na maafisa ustawi wa jamii kushirikiana kwa karibu na wazazi na walezi ili kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata haki yao ya msingi ya elimu.

Sauti ya 3 – Frances Chiwango, Mkurugenzi wa MERODI

Kwa upande wake, Maximilian Makau, mdau wa elimu na mjumbe wa Bodi ya MERODI, ameitaka jamii kuacha kuwaona watoto wenye ulemavu kama mzigo, akisisitiza kuwa wana uwezo wa kujitegemea na kufanikiwa kama watu wengine endapo watapatiwa fursa sawa.

Sauti ya 1 – Maximilian Makau, Mdau wa Elimu na Mjumbe wa MERODI

Makau pia ameitaka serikali kuwaangalia kwa jicho la pekee wazazi wenye watoto wenye ulemavu, hususan kwa kuwawezesha kupitia mikopo au programu maalumu kama ilivyo kwa makundi mengine maalumu, ili kuwasaidia watoto hao kupata elimu bora.

Sauti ya 2 – Maximilian Makau, Mdau wa Elimu na Mjumbe wa MERODI
Share:

Polisi Mtwara wachunguza tukio la mtoto kujaribu kuua

 

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara ACP Issa Suleiman akitoa taarifa ya matukio mbalimbali ya kihalifu kwa waandishi wa habari yaliyotokea mkoani Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linachunguza tukio la mtoto wa miaka 12 anayedaiwa kujaribu kumuua mtoto wa miaka 4 wilayani Nanyumbu. Wakati huo huo, polisi wamefanikiwa kukamata watuhumiwa wa nyara za serikali na dawa za kulevya katika oparesheni mbalimbali mkoani humo.

Na Musa Mtepa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linaendelea kuchunguza tukio la mauaji lililohusisha mtoto, lililotokea katika kijiji cha Masyalele, wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Januari 27, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Issa Suleiman, amesema mtoto Shabani Muebo (12) anadaiwa kujaribu kumuua mtoto mwenzake Ibrahimu Salumu Kelvine (4), wote wakazi wa kijiji cha Masyalele.

ACP Suleiman amesema tukio hilo lilitokea tarehe 23 Januari, 2026, ambapo mtuhumiwa alimlaghai mhanga aliyekuwa akicheza na watoto wenzake, kisha akaelekea naye katika msitu wa jando wa kijiji hicho na kumjeruhi shingoni kwa kutumia kiwembe kabla ya kumtelekeza katika pori.

Kamanda huyo ameongeza kuwa, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina wa tukio hilo, huku mtoto aliyedhurika akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Ndanda, wilayani Masasi mkoani Mtwara.

Sauti ya 1 – ACP Issa Suleiman, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara

Katika hatua nyingine, ACP Suleiman amesema kupitia doria na misako inayoendeshwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa Wanyamapori, watuhumiwa wawili wamekamatwa kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali aina ya meno ya tembo.

Watuhumiwa hao ni Ignas Aron Mponzi (37), mwalimu wa Shule ya Msingi Namitende, na Dickson Ado (46), mkulima, wote wakazi wa kijiji cha Nangumbu wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

 Sauti ya 3 – ACP Issa Suleiman, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara

Vilevile, katika mwendelezo wa oparesheni za kupambana na uhalifu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara tarehe 17 Januari, 2026, liliwakamata Abas Mohamed Nakiti (49) na Mohamedi Mohamed Nakiti (22), wakulima na wakazi wa kijiji cha Mkachima wilayani Masasi, wakiwa na viroba kumi (10) vya dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa jumla wa kilogramu 110.

Sauti ya 4 – ACP Issa Suleiman, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limeeleza kuwa linaendelea kufuatilia na kudhibiti mbinu mbalimbali zinazotumiwa kufanya uhalifu, ikiwemo kupambana na usafirishaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya, ambavyo ni kinyume na sheria za nchi.

Share:

Mtwara wapewa somo unyonyeshaji bora

 

Viongozi na wadau wakiwa kwenye kikao cha Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za TCCIA mjini Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

Jamii Mtwara imehimizwa kunyonyesha watoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo, kuimarisha makuzi yao, huku wadau wakitathmini huduma za malezi na kupanga mipango kupitia PJT-MMMAM.

Na Musa Mtepa

Jamii mkoani Mtwara imetakiwa kuhakikisha watoto wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo bila kuchanganya na chakula au kinywaji kingine chochote, ili waweze kupata makuzi sahihi.

Wito huo umetolewa January 23,2026 wakati wa kikao cha robo mwaka cha wadau mbalimbali wakiwemo  asasi za kiraia kilicholenga kufanya tathmini ya shughuli zilizotekelezwa kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025, pamoja na kupanga mipango kazi ya Januari hadi Machi 2026 kupitia Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za TCCIA mjini Mtwara.

Akizungumza katika kikao hicho, Meneja Mradi kutoka Taasisi isiyo ya Kiserikali ya KIMAS yenye makao makuu yake wilayani Masasi mkoani Mtwara, Torai Kibiti, amesema bado kuna changamoto katika baadhi ya maeneo, ikiwemo uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa mtoto kunyonya maziwa ya mama pekee bila kuchanganya na kitu kingine.

Amesema changamoto hiyo inatokana na imani potofu iliyopo katika jamii kwamba mtoto ambaye hajafikisha miezi sita hawezi kunyonya maziwa ya mama pekee, hali inayohitaji kuongeza juhudi za uelimishaji na hamasa kwa jamii.

Akiwasilisha mada kuhusu chombo cha kupima hali ya utekelezaji na ubora wa utoaji wa huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (Scorecard), kwa niaba ya Ofisa Ustawi wa Mkoa wa Mtwara, Ofisa Ustawi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Godlove Miho, amesema chombo hicho kinasaidia wadau kujitathmini na kubaini ubora wa huduma wanazotoa kwa watoto.

Sauti ya Godlove Miho, Ofisa Ustawi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Vituo vya Kulelea Watoto mkoani Mtwara, Selemani Issa Mkonga, amesema ili kufikia malengo ya Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, jamii haina budi kuwekeza katika uanzishaji wa vituo vya kulelea watoto, kwani idadi iliyopo kwa sasa haitoshelezi mahitaji.

Sauti ya Issa Mkonga, Mwenyekiti wa Vituo vya Kulelea Watoto Mkoa wa Mtwara

Aidha, Issa Mkonga amesema upungufu au kukosekana kwa vituo vya kulelea watoto kumesababisha watoto wengi kukumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo unyanyasaji na vitendo vya ukatili mitaani, na kutoa wito kwa wadau kujitokeza kuanzisha vituo hivyo kwa maslahi ya watoto.

Sauti ya pili ya Issa Mkonga, Mwenyekiti wa Vituo vya Kulelea Watoto Mkoa wa Mtwara

Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM)inalengakuhakikisha watoto wote kuanzia mimba hadi umri wa miaka 8 wanapata malezi, makuzi na huduma bora ili wakuekimwili, kiakili, kihisia na kijamii , ikiwemo Afya na Lishe, Malezi Chanya na Ulinzi wa Mtoto, Elimu ya Awali na Maendeleo ya Akili, Makuzi ya Kihisia na Kijamii na Huduma kwa Watoto Wenye Mahitaji Maalum.

Share:

Vijana kata ya Chuno wahamasishwa kujipanga kiuchumi

 

Baadhi ya vijana wa kata ya Chuno Manispaa ya Mtwara Mikindani wakiwa katika Kongamano lililofanyika Jana January 25,2026 katika ofisi za kata ya hiyo(Picha na Henry Abdala)

Vijana wa Kata ya Chuno, Mtwara Mjini, wametakiwa kuungana katika vikundi ili kunufaika na tenda na mikopo ya serikali kwa maendeleo yao ya kiuchumi

Na Musa Mtepa

Vijana wametakiwa kuungana na kuunda vikundi vitakavyowawezesha kupata tenda na mikopo kutoka serikalini, hatua itakayosaidia kuinua uchumi wao binafsi na jamii kwa ujumla.

Wito huo umetolewa tarehe 25 Januari, 2026 na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Mtwara MjiniNdugu Nassoro Mohemedi, wakati wa Kongamano la Vijana lililofanyika katika Kata ya Chuno.

Akizungumza katika kongamano hilo, Ndugu Mohemedi amesema kuwa vijana wana uwezo wa kujijenga kiuchumi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja iwapo watajipanga vizuri na kutumia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri, sambamba na shughuli zao za kila siku.

Sauti ya Nassoro Mohamedi Mwenyekiti UVCCM Mtwara Mjini

Kwa upande wao, baadhi ya vijana waliohudhuria kongamano hilo wamesema wamejifunza mambo mbalimbali, ikiwemo kutambua fursa zilizopo katika maeneo yao. Aidha, wamewapongeza viongozi wa kata hiyo kwa kuwaandalia kongamano hilo lenye manufaa makubwa kwa maendeleo yao.

Sauti ya baadhi ya vijana wa kata ya Chuno

Naye mratibu wa kongamano hiloIddi wa Mangongo, kwa kushirikiana na Diwani wa Kata ya Chuno, amesema kuwa lengo kuu la kufanyika kwa kongamano hilo ni kutokana na kutambua kuwa vijana ni kundi kubwa na muhimu katika jamii, hivyo wanapaswa kuelimishwa na kupewa taarifa kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika maeneo yao.

Sauti ya Iddi wa Mangongo mratibu wa Kongamano
Share:

Wazazi wahimizwa kulea watoto kimaadili kuzuia mimba kwa wanafunzi

 

Baadhi ya wazazi wa kijiji cha Nanguruwe wakishiriki kipindi cha wazi juu ya ni kifanyike ili kutekeleza mimba kwa wanafunzi (Picha na Henry Abdala)

Wazazi wa kijiji cha Nanguruwe wameaswa kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kukabiliana na mimba kwa wanafunzi. Wito huo umetolewa na viongozi wa elimu, polisi na walimu kupitia kipindi cha Wazi cha Jamii FM Redio.

Na Musa Mtepa

Wazazi wameshauriwa kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi, ikiwemo mimba za utotoni zinazosababisha baadhi yao kusitisha masomo wakiwa shuleni.

Ushauri huo umetolewa na Afisa Elimu Kata ya Nanguruwe, Omari Makiluli, aliposhiriki kipindi cha Wazi kinachorushwa na Jamii FM Redio tarehe Januari 17, 2026. Kipindi hicho kilifanyika katika eneo la stendi ya magari kijijini Nanguruwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.

Akichangia mada iliyokuwa ikijadiliwa ya “Nini kifanyike ili kutekeleza sera na mikakati ya serikali juu ya kutokomeza mimba kwa wanafunzi”Makiluli amesema kumekuwepo na ombwe kubwa la wazazi na walezi katika kuwafuatilia mienendo ya watoto wao. Ameeleza kuwa ni muhimu wazazi kuwa karibu na watoto wao na kuwakuza katika maadili mema ili kuwaepusha na vishawishi vinavyoweza kuathiri maisha yao ya kielimu.

Sauti ya 1: Omari Makiluli, Afisa Elimu Kata ya Nanguruwe

Aidha, Afisa Elimu huyo amewasisitiza wazazi kuwahimiza watoto wao, hususan wa kike, kuendelea na masomo kwa kuhakikisha wanakwenda shule na kupata elimu itakayowawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha zinazojitokeza katika jamii.

Sauti ya 2: Omari Makiluli, Afisa Elimu Kata ya Nanguruwe

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nanguruwe, Mwalimu Keneth Kawinda, amesema kuwa ili kukabiliana na tatizo la mimba kwa wanafunzi, wazazi wanapaswa kuamini kuwa hosteli ni maeneo salama kwa watoto wao. Aidha amewataka wazazi kutoacha watoto wao uhuru wa kujiamulia kufanya mambo yasiyofaa bila usimamizi.

Sauti ya Mwalimu Keneth Kawinda, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nanguruwe

Naye Afisa wa Jeshi la Polisi Kata ya Nanguruwe, WPO Titus Julius Godfrey, amesema utekelezaji wa sera na mikakati ya serikali juu ya kuondoa mimba kwa wanafunzi unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walimu na wanafunzi wenyewe ili kuzungumza lugha moja na kumsaidia mtoto kufikia malengo yake ya kielimu.

Sauti ya WPO Titus Julius Godfrey, Afisa wa Jeshi la Polisi Kata ya Nanguruwe

Kwa upande wao, baadhi ya wazazi na wananchi waliohudhuria kipindi hicho wamekiri kutokuwa karibu vya kutosha na watoto wao, huku wengine wakiahidi kuanza upya kwa kuzungumza na watoto wao kuhusu umuhimu wa elimu na njia za kujiepusha na mimba wakiwa shuleni.

Sauti ya wazazi na wananchi wa Kijiji cha Nanguruwe

Kipindi cha Wazi kinachoratibiwa na Jamii FM Redio kilianza rasmi Oktoba 9, 2025 katika Kata ya Naliendele, Manispaa ya Mtwara Mikindani, kikiwa na mada isemayo “Nini kifanyike ili jamii ishiriki kikamilifu kupunguza tatizo la mimba kwa wanafunzi shuleni”, Januari 17, 2026 kimefanyika katika Kijiji cha Nanguruwe, Halmashauri ya wilaya ya Mtwara kilichokuwa na mada isemayo “Nini kifanyike ili kutekeleza sera na mikakati ya serikali kuzuia mimba kwa wanafunzi shuleni”, huku kipindi kijacho kinachotarajiwa kufanyika Januari 24, 2026 katika Kijiji cha Majengo, Kata ya Ziwani, kikijadili mada ya “Nini kifanyike ili shughuli za kiuchumi zisiwe chanzo cha wanafunzi kupata mimba na kuacha shule”.

Lengo kuu la vipindi hivi ni kutoa elimu kwa jamii, kuhimiza uwajibikaji kwa kila mmoja na kumwezesha mwanafunzi, hususan mtoto wa kike, kutimiza malengo yake kupitia elimu.

Share:

Wananchi wa Nanguruwe waomba msaada ujenzi wa Soko

 

Tofali zikiandaliwa kwa ajili ya ujezni wa Jengo la utawala la soko la kijiji cha Nanguruwe (Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wa kijiji cha Nanguruwe wameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kusaidia ujenzi wa soko la kisasa la bidhaa na vyakula ili kuboresha huduma za kibiashara. Ujenzi huo unafanywa kwa nguvu za wananchi na unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 70, huku wafanyabiashara zaidi ya 100 wakinufaika

Na Musa Mtepa

Wananchi wa kijiji cha Nanguruwe wameiomba Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kuchangia na kusaidia ujenzi wa soko la bidhaa na vyakula unaoendelea kujengwa katika kijiji hicho.

Wakizungumza na Jamii FM Redio Januari 17, 2026, wananchi hao wamesema kuwa kutokana na ukuaji wa kasi wa kijiji chao, viongozi wa kijiji wameamua kuanzisha ujenzi wa soko la kisasa ili kuwaondolea adha wakazi wa kijiji hicho kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kibiashara eneo la Barabarani.

Sauti ya wananchi wa kijiji cha Nanguruwe
Eneo linalotarajiwa kujengwa kwa soko la kijiji cha Nanguruwe (Picha na Musa Mtepa)

Akizungumza kuhusu ujenzi wa soko hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nanguruwe, Bw. Saidi Mandova, amesema kuwa sababu kubwa ya uamuzi huo ni matumizi ya soko moja kwa vijiji vitatu kwa muda mrefu, hali iliyokuwa ikikisababishia kijiji kukosa mapato yatokanayo na shughuli za kibiashara.

Bw. Mandova ameongeza kuwa ujenzi wa soko hilo unatekelezwa kwa nguvu za wananchi wenyewe, huku akiomba wadau wa maendeleo kujitokeza kusaidia ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Sauti ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nanguruwe

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Nanguruwe, Bw. Saidi Hamisi, ameelezea hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo na kufafanua kuwa ujenzi unaendelea vizuri licha ya changamoto chache za upungufu wa rasilimali.

Ameongeza kuwa hadi kukamilika, ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 70, huku zaidi ya wafanyabiashara 100 wakitarajiwa kunufaika na huduma za soko hilo.

Sauti ya Afisa Kaimu Mtendaji wa kijiji cha Nanguruwe
Eneo lililopangwa kwa ajili ya kujenga vibanda vya Wafanyabiashara katika soko la kijiji cha Nanguruwe(Picha na Musa Mtepa)
Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>